TAKUKURU YAWAHAMASISHA WENYE ULEMAVU KUJITOKEZA KUWACHAGUA VIONGOZI WANAOWEZA KUTETEA MASLAHI YAO

 




Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 wa kuwachagua Madiwani, Wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro imewahamasisha watu wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaoweza kutetea maslahi na maendeleo yao.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo ya utoaji elimu dhidi ya rushwa kwa viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu na mahitaji maalum mkoani humo, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro, Bw. Christopher Mwakajinga, amesema ushiriki wa kundi hilo katika uchaguzi si hisani bali ni haki yao ya msingi inayotokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Ushiriki wa watu wenye mahitaji maalum kwenye uchaguzi ni haki ya kikatiba, si fadhila. Ni lazima tuweke mazingira huru na sawa ili waweze kuitumia haki yao ya kupiga kura,” amesema Mwakajinga.


Amefafanua kuwa Katiba ya nchi inatoa haki ya kushiriki katika uongozi kwa Watanzania wote waliotimiza umri wa miaka 18 bila kujali hali zao za kimwili, kiuchumi au kijamii, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kutumia haki hiyo kwa uhuru.

Aidha, baadhi ya viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu wamewasihi wenzao wasishawishike na zawadi au rushwa za uchaguzi, bali watumie busara na uelewa wao kuchagua viongozi watakaotetea maslahi ya watu wenye ulemavu, kudumisha amani na kuendeleza maendeleo ya Taifa.

No comments:

Post a Comment